Uhuru Wa Vyombo Vya Habari Kuangaziwa Duniani Kote
Taarifa potovu, matamshi ya chuki na mashambulizi mabaya dhidi ya waandishi wa habari yanatishia uhuru wa vyombo vya habari duniani kote ndio kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa wito wa umoja.
Wito huo unajiri wakati wa kuelekea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Mei, kulingana na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la 1993.
Lengo mwaka huu ni juu ya uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu kwa ujumla.
Waandishi wa habari mashuhuri na wakuu wa vyombo vya habari na mashirika ya haki za binadamu kutoka duniani kote wanahudhuria tukio hilo, wakibadilishana uzoefu na maoni yao katika majopo kadhaa kuhusu masuala kama vile mataifa mengi na uhuru wa kujieleza.
Akitoa hotuba ya ufunguzi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni UNESCO, Audrey Azoulay, linalotetea ulinzi wa wanahabari, alisema mwaka 2022 ndio mwaka wa hatari zaidi kwa taaluma hiyo.
Mwaka jana, waandishi wa habari 86 waliuawa, hasa nje ya maeneo ya vita. “Mara nyingi, walikuwa nyumbani na familia zao,” alisema. Mamia zaidi walishambuliwa au kufungwa.
Zaidi ya hayo, waandishi wa habari pia wanashambuliwa katika anga ya mtandao.
Ripoti ya 2021 ilifichua kuwa wanahabari watatu kati ya wanne wanawake wamekuwa waathiriwa wa unyanyasaji mtandaoni, na kusababisha UNESCO kutoa mapendekezo kwa majukwaa ya kidijitali kuongeza ulinzi.
Azoulay alibainisha kuwa changamoto hizi zinatokea wakati ambapo wanahabari wanahitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kwani ujio wa enzi ya kidijitali umebadilisha hali nzima ya habari.
Ingawa Mtandao umefungua njia mpya za habari na kujieleza, pia umetoa msingi mzuri kwa wale wanaotaka kupanda habari potofu na nadharia za njama. ‘Njia panda mpya’
Aidha Alitoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi ili kuhakikisha kuwa taarifa zinaweza kubaki kuwa manufaa ya umma, akibainisha kuwa UNESCO inaunga mkono baadhi ya nchi 20 kuunda sera za elimu katika vyombo vya habari na ujuzi wa habari katika enzi ya digitali.
Shirika hilo pia liliandaa mkutano mkubwa wa kimataifa mjini Paris mwezi Februari ili kujadili rasimu ya miongozo ya kimataifa ya kudhibiti mifumo ya kidijitali, ambayo itachapishwa baadaye mwaka huu.
Katika hotuba yake kuu, Sulzberger, Mwenyekiti na Mchapishaji wa The New York Times, alionyesha wasiwasi wake juu ya jinsi vitisho vya uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni pote vinaathiri mfumo wa kimataifa.
Sulzberger alitafakari jinsi mandhari ya vyombo vya habari yamebadilika tangu 1993 – kipindi cha matumaini kinachojulikana na mwisho dhahiri wa mgawanyiko wa Vita Baridi, kuibuka kwa demokrasia changa, na maendeleo ya teknolojia katika habari na muunganisho.
Hata hivyo Alisema muda huo ni wa muda mfupi kwani teknolojia iyo hiyo iliyowawezesha waandishi wa habari kuwafikia watu kila mahali pia ililazimisha maelfu ya magazeti kufungwa, na vyombo vya habari vya kidijitali vilivyoibuka havikuweza kujaza pengo hilo, hasa katika kutoa taarifa muhimu za ndani na za uchunguzi.
Pia aliangazia kesi ya mwandishi wa Wall Street Journal Evan Gershkovich, ambaye alikamatwa huko Yekaterinburg mwezi uliopita kwa madai ya ujasusi, akisema mwandishi huyo wa zamani wa Times “anaendelea kuzuiliwa na Urusi kwa mashtaka ya uwongo na anapaswa kuachiliwa.”
Sulzberger aliambia Mataifa Wanachama wa Umoja wa Mataifa kwamba kukabiliana na shambulio la kimataifa kwenye vyombo vya habari kutatatuliwa tu ikiwa watachukua hatua.
Aidha alisisitiza haja ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kuandaa mifumo ya wazi ya kifedha kwa ajili ya kuendeleza uandishi huru wa habari.