Sabina Chege Apinga Raila
Mbunge mteule wa Jubilee Sabina Chege amewapuuza viongozi wa upinzani kwa wito wao wa kurejelea maandamano siku ya Jumanne.
Chege alisema yuko tayari kupoteza nafasi hiyo badala ya kuunga mkono maandamano yaliyopangwa na muungano wa Azimio-One Kenya.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukaribisha nyumbani kwa mwakilishi wadi wa Kanyenyaini Grace Nduta, Chege alisema kuwa ni wakati wa Wakenya kufanya kazi na kupunguza changamoto zinazoikabili nchi badala ya kupoteza muda katika maandamano.
Chege alitoa wito kwa viongozi hao kukubaliana na kushiriki mazungumzo yatakayosuluhisha baadhi ya matatizo na masaibu yanayokumba Wakenya.
Maoni yake yaliungwa mkono na Mbunge wa Juja George Koimburi aliyewataka viongozi wa upinzani kusitisha maandamano yaliyopangwa na kutoa fursa kwa majadiliano hayo ya pande mbili.
Kwa upande wake, Mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel Kagombe alimtaka Rais wa zamani Uhuru Kenyatta kujiepusha na siasa kali na kujihusisha na masuala ambayo yataleta amani katika nchi zilizokumbwa na vita barani Afrika.
Mbunge wa Kandara Chege Njuguna alisisitiza kuwa serikali inalenga kufufua uchumi unaodorora akisema hawataketi kutazama mali ya watu ikiharibiwa wakati wa maandamano.
Wakati uo huo, viongozi hao walisema hawatachoka na madai yao ya kuwa na fomula ya mtu mmoja shilingi moja katika kugawana mapato.
Kaunti za eneo la kati, waliteta kwamba zimeathiriwa pakubwa na mbinu ya nchi ya kugawana rasilimali na serikali ya kitaifa ikizingatia idadi kubwa ya watu wa eneo hilo.