Raila Asisitiza Maandamano Yataendelea Kesho

Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja One-Kenya Raila Odinga anasema maandamano ya kupinga serikali yaliyopangwa kufanywa na upinzani bado yatafanyika Jumanne licha ya polisi kukataa kuwaruhusu.
Kupitia taarifa ya Jumapili, Odinga ameshikilia kuwa upinzani unatumia haki yao ya kikatiba ya kukusanyika, kuandamana, na kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka za umma kwa amani.
Kutokana na hayo, ametangaza kwamba watawasilisha maombi katika afisi nne za serikali Jumanne katika juhudi za kushinikiza utawala wa Rais William Ruto kutii matakwa yao.
Odinga, ambaye amekataa kukubali kushindwa na Dkt rais william Ruto katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 2022, amesema watawasilisha ombi kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuthibitisha madai yao kwamba matokeo ya uchaguzi yalithibitishwa na kutaka ukaguzi wa seva za uchaguzi.
Kulingana na Odinga, pia wataelekea katika Hazina ya Kitaifa kuomba fedha zote zinazodaiwa kaunti ziachiliwe mara moja na kulipwa mishahara kwa wakati kwa wafanyikazi wote wa umma.
Odinga alisitisha maandamano ya kila wiki ya Aprili 2, baada ya Rais Ruto kumkaribisha Odinga kwenye mazungumzo ya pande mbili za bunge kushughulikia malalamishi yao.
Lakini mchakato huo haujafua dafu, huku upinzani ukishutumu timu ya Kenya Kwanza kwa kushindwa kujitolea kufanya mazungumzo yenye kujenga.