Daktari Amoth Kuendelea Kuhudumu Kama Kaimu Mkurugenzi Mkuu Wa Afya
Dkt. Patrick Amoth ataendelea kuhudumu kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya, kulingana na mabadiliko kadhaa yaliyotangazwa na Waziri wa Afya Susan Wafula.
Tangu 2019, Amoth, ambaye pia anahudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya Shirika la Afya Ulimwenguni, amehudumu kama mshauri mkuu wa kiufundi wa serikali kwa uhusiano na Wizara ya Afya.
Muda wake wa zaidi ya miaka minne katika nafasi hiyo umezua mjadala tangu achukue wadhifa huo kutoka kwa Dk John Masakabi.
Mnamo Machi 2022, Waziri wa Afya wa wakati huo Mutahi Kagwe aliitwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Afya kueleza ni kwa nini Amoth alikuwa bado hajateuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Kulingana na Kagwe, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilichelewesha kuidhinisha mapendekezo ya muundo wa shirika na uanzishaji wa wafanyikazi ili kujaza nafasi hiyo.
Bado haijulikani kwa nini Dkt. Amoth hakuthibitishwa kamwe kuwa Mkurugenzi Mkuu, huku PSC ikiongeza fumbo kwa kutangaza nafasi yake mnamo Juni 2022.
Wakati uo huo katika mabadiliko mapya katika Wizara ya Afya, Waziri Susan Nakhumicha amewataja manaibu wakurugenzi wakuu wawili wapya,, Dkt Zainab Gura atakuwa naibu mkurugenzi mkuu wa Idara ya Huduma za Matibabu na Dkt Sultani Matendechero kama naibu mkurugenzi mkuu wa Afya ya Umma na Viwango vya Kitaalamu.
Dkt Andrew Mulwa amehamishiwa Kurugenzi ya Afya ya Familia, huku Joseph Tunai akichukua nafasi yake katika Kurugenzi ya Kinga na Afya.
Katika mabadiliko hayo mapya, Irene Inwani atasimamia Kurugenzi ya Huduma za Kliniki, na Elizabeth Wangia atasimamia ile ya Ufadhili wa Afya.
Dkt. Francis Kuria amebakishwa kama Mkurugenzi wa Afya ya Umma na Usafi wa Mazingira.
Kulingana na mabadiliko yaliyotangazwa ,maafisa hao watahudumu kama kaimu kuanzia Aprili 19, 2023.