Gachagua Azungumzia Mwanya Uliopo Katika Mazungumzo Ya Pande Mbili
Naibu Rais Rigathi Gachagua ameshikilia kuwa Rais William Ruto ataingilia tu mazungumzo hayo ya pande mbili iwapo suala lolote muhimu litatokea.
Akiwahutubia viongozi wa Kiislamu katika ukumbi wa KICC, Gachagua amebainisha kuwa kamati hiyo ya wanachama 14 ilikuwa imepewa jukumu la kushughulikia masuala yaliyotolewa na pande zote mbili na akaeleza imani kwamba timu iliyochaguliwa itatekeleza majukumu yake.
Gachagua aliongeza kuwa Rais atajikita katika kufufua uchumi licha ya wito wa Azimio wa mazungumzo
Kuhusiana na vitisho vya Azimio kurejea barabarani, Gachagua amesisitiza kuwa serikali iko tayari kukabiliana na maandamano hayo akibainisha kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya wanaoharibu mali.
Aidha Azimio imetoa wito kwa umma kushirikishwa katika mazungumzo hayo.
Timu inayoongozwa na Raila ilibaini kuwa baadhi ya masuala yanahitaji sauti ya Wakenya.
Wakati huo huo, kivumbi kinatarajiwa katika kamati ya pande mbili baada ya timu ya Kenya Kwanza kukataa baadhi ya masuala ambayo yaliibuliwa na Azimio ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa sava na kurejeshwa kazini kwa waliokuwa makamishna wanne wakiongozwa na Juliana Cherera.
Timu ya Kenya Kwanza itaongozwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale huku timu ya Azimio ikiongozwa na Seneta wa Narok Leadma Ole Kina.