Home » Chama Cha Wazazi: Shule Zinahatarisha Maisha Ya Wanafunzi Kwa Kuajiri Wauguzi Wasiohitimu

Chama Cha Wazazi: Shule Zinahatarisha Maisha Ya Wanafunzi Kwa Kuajiri Wauguzi Wasiohitimu

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wazazi Silas Obuhatsa ameshutumu wasimamizi wa shule kwa kuajiri wauguzi wasiohitimu, na hivyo kuweka maisha ya wanafunzi hatarini.

 

 

Akihojiwa na Kituo kimoja cha redio humu nchini, kiongozi huyo aliyetoa kauli hiyo ameitaka serikali kuchukua hatua haraka na kuunda jopokazi litalokachochunguza uwezo wa watumishi wote wasio walimu shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama.

 

 

Kauli hiyo inajiri baada ya wanafunzi wawili wa shule ya “The Sacred Heart Mukumu Girls” katika kaunti ya Kakamega kufariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na usafi, huku mamia wakilazwa muda mfupi kabla ya shule hiyo kufungwa kwa muda usiojulikana.

 

Serikali ilihusisha mlipuko wa ugonjwa huo shuleni na uchafuzi wa maji.

 

Katika muda wa chini ya wiki moja, Shule ya Upili ya Wavulana ya Butere katika kaunti hiyo pia ilifungwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa, ambao sasa unachunguzwa baada ya wanafunzi kulalamikia kuumwa sana na tumbo na kuendesha.

 

Akijibu kufungwa kwa shule hizo mbili, Obuhatsa anasema kuwa matukio hayo yanaakisi hali duni ya usafi wa mazingira shuleni, na kwamba ni lazima washikadau kubuni mikakati ya kuzuia majanga yajayo.

 

Mwenyekiti huyo wa chama pia amependekeza ianzishwe hospitali katika kila shule ili wanafunzi wapate Huduma ya Kwanza na zingine.

 

Aidha, anadai kuwa idadi ya vifo vinavyoripotiwa shuleni kutokana na maradhi huenda ikapungua iwapo shule zitakuwa na hospitali zinazoweza kushughulikia masuala madogo madogo yanayowakabili wanafunzi huku akitolea mfano kuwa shule nyingi ziko mbali na hospitali hali inayoweka maisha ya wanafunzi hatarini.

 

Hata hivyo, mwenyekiti huyo pia amewasuta maafisa wa Wizara ya Elimu kwa kushindwa kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha shule zinazingatia viwango vya usalama na usafi wa Wizara.

 

Kadhalika, amewaonya wasimamizi wa shule dhidi ya kuwarudisha wanafunzi nyumbani bila kuwajulisha wazazi wao au kukosa kuwaarifu wazazi pindi mwanafunzi anapougua kwa wakati.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!