Wapenzi Wa Lugha Ya Kiswahili Walitembelea Kaburi La Prof. Ken Walibora
Tarehe 10, April 2020 itasalia tarehe ya kumbukizi na majonzi miongoni mwa wapenzi wa Lugha ya Kiswahili nchini Kenya.
Ni siku ambayo wafia lugha ashirafu ya Kiswahili siyo tu nchini Kenya bali duniani kote katu hawatoisahau.
Kwa uwepo wa janga la UVIKO- 19, wafia lugha walitamani ardhi ipasuke wayatafute mauti, wayavamie na kuyaua lakini yote yalikuwa ruiya.
Kifo chake mtoto wa mwalimu jina rasmi Ken Waliaula au kwa wengi Profesa Ken Walibora, kiliwaacha kwenye huzuni mwaka elfu mbili na ishirini.
Kama tu Marehemu Sheikh Shaaban Roberts wa Tanzania, ndivyo alivyokuwa Profesa Walibora nchini Kenya.
Siku ya Jumamosi, tarehe 8 mwezi wa April 2023, wapenzi na wafia lugha ashrafu ya Kiswahili wamekongamana nyumbani kwake Profesa Ili kumuaga rasmi.
Kwa uwepo wa virusi vya korona nchini mwaka elfu mbili na ishrini na moja, mashabiki, wafuasi, magwiji na wapenzi wa Kiswahili hawakuweza kwenda kumuaga.
Hili lilichochewa zaidi na sheria kali zilizowekwa nchini kudhibiti maambukizi na maenezi ya virusi hivi vya korona kama watu kuwekwa karantini, kudhibiti idadi ya watu kujumuika na pia kafyu.
Mwaka elfu mbili na ishrini na mbili, mbio mbio na mihemko ya siasa ilitibua mpango wa sherehe za kumbukumbu kwake Profesa Walibora.
Licha ya kuwepo kwa changamoto hizo, wafia lugha wamevalia magwanda ya fasihi hadi Gatuzi la Trans Nzoia, eneo bunge la Chereng’anyi, Makutano Kwa Ngozi alikozikwa Walibora.
Marehemu Walibora kabla ya kifo chake, alihudumu kama mwanahabari Kampuni ya Nation kwenye vituo vya; Qtv, Qfm, NTV, Daily Nation na Gazeti la Taifa Leo.
Zaidi ya hilo, alikuwa mwandishi wa riwaya, hadithi fupi, tamthilia na makala maalum ya utafiti wa fasihi.
Mojawapo ya Riwaya yake pendwa Siku Njema, ilitahiniwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1996 nchini Kenya kama Riwaya ya kwanza ya mkenya kutahiniwa nchini.
Aliandika vitabu vingine kama; Tamthilia ya Mbaya Wetu, Riwaya ya Kidagaa Kimemwozea miongoni mwa kazi nyingi za kifasihi.
Wakati wa kifo chake mjini Nairobi, Walibora alikuwa mhadhiri Chuo Kikuu cha Riara na pia, baba wa wana wawili wanaoshi Marekani.
Jumamosi hii kikosi cha wafia lugha kimeongozwa na Hassan Bin Muchai (Chui), Hassan Mwana wa Ali (Amope) miongoni mwa wengi Ili kufanikisha shughuli ya kumuomboleza Walibora.
Kulingana na mwanahabari mkongwe na tajika wa Taifa Leo, Hassan Muchai, wafia lugha ya Kiswahili zaidi ya 300 watarajiwa kufika Makutano Kwa Ngozi, Chereng’anyi. Mola aendelee kuilaza roho yake Profesa Ken Walibora penye wema.