Maisha Magumu Yawageuza Wasichana Wa Shule Kuwa Walezi Samburu
Kaunti ya Samburu ni mojawapo ya maeneo yenye ukame nchini ambapo imeathiriwa pakubwa na athari za mabadiliko ya hali ya anga.
Kutokana na kupanda kwa gharama za maisha wazazi ambao ni wazee, wamekatishwa tamaa na umaskini, wasio na kazi au walevi hawawezi kuwaandalia watoto wao chakula.
Mtoto wa kike ndiye ameathirka kwa sababu matarajio ya kitamaduni ya kaunti ya Samburu yanampa mtoto wa kike jukumu makubwa.
Wasichana wengi katika kaunti ya Samburu eneo la Partuk wameacha shule na kwenda katika msitu wa Kirisia kuchoma makaa ambayo huwauzia wenyeji ili kununua chakula cha familia zao.
Kuchoma Mkaa kunaleta hatari kubwa kwa wasichana wadogo kwa sababu msitu huo ni makazi ya tembo ambao wameua watu siku za nyuma.
Aidha wengi Wana umri wa kati ya miaka 15 na 17.
Lempara Elisheba mkazi wa kaunti ya Samburu alisema; “Utakutana na mwanamume katika harakati za kuchoma mkaa wasichana wanakutana na wanaume ambao wanawadanganya kuwa watasaidia kulisha familia zao na kuwanunulia chakula na kwa njia hiyo wakawapa ujauzito,”
Janet Wanjiru, mwanzilishi wa Mpango wa Kuwawezesha Wanawake wa Samburu ambao huwaokoa wasichana kutoka kwa ndoa za utotoni anathibitisha, ‘’kuna mamia na mamia ya akina mama matineja ambao wanaacha shule katika kaunti hiyo,”
Kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya, Kaunti ya Samburu inaongoza kwa mimba za utotoni kwa 50%.
Laisoi, sio jina lake halisi, mwenye umri wa miaka 17, anafichua kwamba aliacha shule akiwa na umri wa miaka 13 ili kuchoma mkaa msituni.
‘’Niliacha shule kwa ajili ya kuchoma na kuuza mkaa ili kuwapa chakula wazazi na ndugu zangu na katika harakati hizo nilipata ujauzito’’.
Sasa ameolewa na ana watoto na kwa sasa ni mjamzito tena. Mume hukaa nyumbani hafanyi chochote kukimu familia kwa vile mifugo iliangamizwa na ukame. Yeye ndiye mlezi pekee wa mume na watoto
Elimu ni haki ya binadamu nchini Kenya. Kifungu cha 53 cha Katiba ya Kenya ya 2010 kinasema kwamba kila mtoto ana haki ya kupata elimu ya msingi bila malipo na ya lazima.
Kukaa nje ya darasa ili kutunza familia zao na kufanya kazi za nyumbani ni ukiukwaji wa haki zao.
Ingawa serikali ya kaunti ilianzisha mpango wa kulisha watoto shuleni ili kuwaweka shuleni ambao ni vigumu kupata mlo nyumbani bado wengi wamesalia nyumbani.