Mke Wa Rais Awaagiza Viongozi Wa Kidini Kuharakisha Mazungumzo
Mke wa Rais, Mama Rachel Ruto, alihudhuria ibada ya maombi ya amani kati ya madhehebu mbalimbali katika Taasisi ya Utafiti wa Misitu ya Kenya huko Marigat, Kaunti ya Baringo.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi mbali mbali zinazofanyika kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro baina ya jamii za wafugaji eneo hilo.
Maombi ya madhehebu yaliyowaleta pamoja viongozi wa dini kutoka kata nne; Baringo, Samburu, Turkana, na Elgeyo Marakwet, walithibitisha hitaji la uwekezaji ambao unabuni ajira mbadala kwa vijana na wanawake, na kupunguza utegemezi kupita kiasi kwa mifugo ili kujikimu kimaisha.
Mama Rachel Ruto alitoa wito wa uwekezaji zaidi katika kilimo, akisema kuwa usalama wa chakula utapunguza mizozo miongoni mwa jamii zinazozozana.
Kaunti 4 zilizowakilishwa katika mkutano huo zimeathiriwa zaidi na ukame wa muda mrefu ambao umesababisha baadhi ya maeneo ya Kenya kukosa mvua kwa zaidi ya misimu 4 mfululizo.
Mke wa Rais aliwahimiza viongozi wa kidini waliohudhuria kutumia majukwaa yao kuhimiza amani kati ya jamii zilizoathiriwa na wizi wa ng’ombe.
Mbinu hii itajenga imani miongoni mwa jamii zilizoathirika na kusababisha suluhu la muda mrefu la amani na utulivu endelevu.