Wakaazi Wa Nairobi Wakadiria Hasara Kutokana Na Mvua Kubwa
Mvua imeendelea kusababisha uharibifu kote nchini huku nyumba na maduka zikifurika, kuharibu mali na kukata njia kwa baadhi ya maeneo.
Jijini Nairobi, baadhi ya wakaazi wamesalia na butwaa baada ya mafuriko kuingia katika nyumba zao na kuharibu vifaa vya elektroniki na vitu vingine.
Huko Eastleigh, maji taka yameonekana kuelea huku wafanyabiashara wakijaribu kuondoa maji kutoka kwa maduka yao.
Katika sehemu za Githurai na Kahawa Wendani, wakaazi wameachwa wakihesabu hasara huku samani zao na vitu vingine vikiharibiwa na mafuriko.
Huko Imara Daima, hali haikuwa tofauti, huku wakazi wakilazimika kuvua viatu na kupita kwenye maji ili kuingia na kutoka maeneo wanakoishi.
Maeneo kadhaa pia yanakabiliwa na kukatika kwa umeme huku mvua zikinyesha jijini Nairobi.
Mtaalamu wa hali ya hewa alikuwa ametabiri kuanza kwa mvua ndefu katika maeneo ya nchi mwishoni mwa juma.
Madereva kadhaa wamekwama katika msongamano wa magari leo Jumamosi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha.