Tanzania Yapokea Mikopo Nafuu Kutoka Benki Kuu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeingia mkataba na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya jumla ya dola za Marekani milioni 550 pamoja na misaada ya jumla ya dola za Marekani milioni 29.93.
Hii ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Afya ya Mama na Mtoto Tanzania pamoja na mpango endelevu wa maji na usafi wa mazingira vijijini.
Hafla ya utiaji saini mikataba hii ilifanyika tarehe 28 Februari 2023 jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Mkataba huu wa mikopo na misaada utawezesha utekelezaji wa mradi wa Mpango Endelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini, ambao utapokea dola za Marekani milioni 300 za mkopo wa masharti nafuu kutoka IDA na dola za Marekani milioni 4.93 kama msaada kutoka Mpango wa Energy Sector Management Assistance Program (ESMAP).
Mradi huu utasaidia kuongeza upatikanaji wa vyanzo vya maji salama hasa katika maeneo yenye upungufu au changamoto ya upatikanaji wa maji vijijini.
Aidha, mkataba huo utawezesha utekelezaji wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto Tanzania, ambao utapokea dola za Marekani milioni 250 za mkopo wa masharti nafuu kutoka IDA na dola za Marekani milioni 25 kama msaada kutoka Mfuko wa Global Financing Facility for Women Children and Adolescents Multi-Donor Trust Fund. Mradi huu utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto nchini.

Mikataba hii inaendana na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26 na Dira ya Zanzibar 2050, na ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolenga kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Madelu Nchemba ametoa shukrani kwa Benki ya Dunia kwa fursa hii na ameeleza kuwa miradi hii italeta maendeleo makubwa kwa watu wa Tanzania. Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya na maji safi na salama.
Huku Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Nathan Belete amesema amesema miradi hiyo miwili ni muhimu kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowkumba Watanzania ikiwemo katika sekta ya afya pamoja na mpango endelevu wa maji na usafi wa mazingira vijijini.