PSC Yatafuta Ufadhili Wa Kuajiri Wakufunzi Wa TVET
Tume ya Utumishi wa Umma PSC inashinikiza ufadhili wa kuajiri wakufunzi wa Elimu ya Ufundi Stadi (TVET’s).
Mwenyekiti wa PSC Anthony Muchiri amewasiliana na Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Leba ili kuangazia ufadhili wa shughuli ya kuajiri ambayo ilihamishwa kutoka Wizara ya Elimu hadi PSC.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Sera ya Bajeti ya 2023 kwa Kamati katika hoteli moja jijini Nairobi, Mwenyekiti wa PSC amesema kwamba mara tu taasisi za TVET’S zinapokuwa na wakufunzi wa kutosha, vijana watafaidika kwa kupata ujuzi wa kiufundi na kujiajiri wenyewe.
Tayari serikali imeweka mikakati ya kuajiri wakufunzi 1,000 kwa shule 144 za TVET.
Wakufunzi 887 watapangiwa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi (T.T.I’s), 79 kwa vyuo anwai vya kitaifa, na 34 kwa taasisi za mahitaji maalum.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais William Ruto alisema nia ya utawala wake ni kuajiri walimu zaidi katika vyuo vya TVET kote nchini.
Mpango wa awali ulikuwa kuajiri wakufunzi 3,000 ili kuziba pengo ambalo kwa sasa liko la wakufunzi 6,500.