Home » Mwanaume Laghai Auawa Tanzania

Mwanaume mmoja anayefahamika kama Majid Mohamed, mwenye umri wa miaka 36  ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi.

 

Mwanaume huyo mkazi wa Tinde mkoani Shinyanga nchini Tanzania, inasemekana aliuawa kwa tuhuma za kudanganya kuwa yeye ni wakala wa mabasi kisha kuwavamia na kuwaibia mali zao.

Akieleza juu ya tukio hilo, Diwani wa Kata ya Tinde, Jafari Makwaya, amesema tukio hilo lilitokea Februari 21, 2023 majira ya saa nane usiku katika kitongoji cha Jomu Kata ya Tinde Mkoani Shinyanga, ambapo mwanaume huyo alikuwa amewavamia wanawake wawili kwa lengo la kuwaibia ila mlinzi wa malori barabarani na madereva malori walifanikiwa kuwaokoa wanawake hao.

 

“Alipigwa akiwa kwenye shughuli za kuwavamia watu lakini dereva wa lori na mlinzi wa malori walishuhudia tukio zima ambapo walienda kutoa msaada kwa wanawake wale kisha wakamvizia Majid Mohamed akiwa anakimbia kisha kumpiga na kitu chenye ncha kali na kumtupia kwenye mfereji wa barabarani”, amesema Makwaya.

“Alikuwa anawadanganya watu kuwa ni wakala wa mabasi na ni mzawa wa Tinde na amewahi kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la ubakaji na wizi wa madawa ya hospitali na baada ya kutoka gerezani alianza kutishia maisha watu waliofuatilia kesi ,kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana kazi katika kata hii hivyo niombe kwa vyombo vya ulinzi na usalama kushughulika na vijana wanaowadanganya watu na kuwaibia kwa kimvuli cha uwakala”, ameongeza.

Inaelezwa kuwa kijana huyo anayedaiwa kuwa kibaka maarufu amekuwa tishio katika eneo la Tinde kutokana na vitendo vyake huku wananchi wakidai amekuwa akikingiwa kifua hivyo kutofungwa jela.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!