Ongezeko La Visa Vya TB Kaunti Ya Uasin Gishu Vyazidi

Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu kupitia Idara ya Huduma za Afya imeripoti ongezeko la visa ugonjwa wa TB, idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea.
Kulingana na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Kaunti ya Huduma za Afya Dkt. Sam Kotut, watu elfu 1,907 waliopimwa kufikia Desemba mwaka jana walipatikana na maambukizi ya TB.
Hii ni licha ya hatua zilizowekwa na kitengo kilichogatuliwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Dkt Kotut amekuwa akizungumza mjini Eldoret wakati wa uzinduzi wa zoezi la mwezi mmoja la uchunguzi bila malipo ambalo litafanywa katika vituo vyote vya afya vya kaunti.
Ametaja ongezeko la visa vilivyoripotiwa na mwamko mpya katika maeneo ya vijijini na watu wengi kupimwa.
Aidha amedai kaunti imeongeza maradufu bajeti ya dawa na uchunguzi wa magonjwa hadi shilingi. milioni mia 200 kutoka kwa takwimu ya awali ya shilingi. Milioni mia 100 ili kuafikia viwango vya magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Aidha Kotut amewataka wakazi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upimaji bure akisema watakaobainika kuwa na maambukizi watatibiwa bure na kupewa taarifa za jinsi ya kutowaambukiza wengine.
Siku ya Kifua Kikuu Duniani mwaka huu itaadhimishwa huko Uasin Gishu mnamo Machi 24, 2023.