Serikali Ya Kisumu Yamfikisha Mahakamani Padre John Pesa
Serikali ya Kaunti ya Kisumu, kupitia idara ya afya ya umma, imemshtaki kasisi mwenye utata John Juma Pesa wa Kanisa la (Holy Ghost Coptic Church of Kenya) kwa kuwashikilia kinyume cha sheria watu wenye matatizo ya kiakili katika hali mbaya.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Winam, Fatuma Rashid ameagiza mawakili wa pande zote mbili wawasilishe majibu kufikia Alhamisi na kwamba usikilizwaji utaanza Ijumaa tarehe 27 mwezi huu kwa kuwa kesi hiyo imethibitishwa kuwa ya dharura.
Kulingana na taarifa ya mahakama, idara ya afya inasema watu 23 wenye matatizo ya kiakili wanazuiliwa katika kanisa hilo kando ya barabara kuu ya Kisumu-Kakamega lakini wanakosa huduma za kimsingi kama vile vyoo ambavyo ni hatari kwa afya ya umma na ni kinyume cha Sheria ya Afya ya Umma.
Wakili wa kasisi huyo hapo awali aliambia mahakama kwamba mteja wake alihitaji muda zaidi kuangazia ombi hilo kutoka kwa idara ya afya ya umma kwani walipokea tu Jumanne asubuhi.
Idara ya afya ya umma ambayo iliwakilishwa na Wycliffe Owuor, mkuu wa afya ya umma pia iliambia mahakama kuwa suala hilo ni la dharura na halingeweza kusubiri kutokana na hali ambayo wagonjwa wanaishi wanahitaji matibabu ya dharura.
Fredrik Moi, afisa wa afya ya umma katika kaunti ndogo ya Kisumu ya kati ambaye alizungumza na wanahabari baada ya kikao cha mahakama anasema wanatumai mahakama itatekeleza haki haraka ili kuwawezesha wanaozuiliwa kanisani kupata huduma bora za afya