Nchi za Afrika Mashariki Kutumia Sarafu Moja

Daktari Peter Mathuki, Katibu Mkuu EAC
Nchi saba zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kuwa na sarafu moja
na vile vile Benki Kuu ya Afrika Mashariki hivi karibuni iwapo baraza la mawaziri
litapitisha pendekezo hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki, mawaziri hao wanatarajiwa kutoa
uamuzi hivi karibuni kuhusu eneo la Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki, mtangulizi
wa Benki Kuu ya Afrika Mashariki itakayotoa sarafu hiyo moja.
Mathuki ameongeza kuwa biashara kati ya nchi wanachama imeimarika,
ambapo thamani ya biashara ya ndani ya EAC mwaka jana ilifikia dola bilioni 9.5
ikilinganishwa na dola bilioni 7.1 mwaka 2019.
Mathuki alihusisha ongezeko la biashara ya ndani ya kanda na nia njema
ya kisiasa miongoni mwa wanachama.
Akiikubali Somalia katika EAC, Mathuki amesema wanatuma ujumbe wa uhakiki nchini
Somalia ambao utafanya tathmini ya utayari wa nchi hiyo kujiunga na jumuiya hiyo
mwishoni mwa mwezi huu.
Mathuki alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Machakos ambapo alikuwa akielezea
maeneo ya kipaumbele ambayo jamii itaangazia 2023.