Home » Mbunge Mbui Aisuta Serikali

Mbunge wa Kathiani Robert Mbui ameisuta serikali ya Kenya Kwanza kwa kukaidi maagizo ya mahakama baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Petroli (EPRA) kuongeza bei ya mafuta.

 

Hii ni licha ya agizo la Mahakama Kuu kusitisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023, ambayo miongoni mwa mapendekezo mengi, inataka nyongeza ya ushuru kwenye mafuta kutoka 8% hadi 16%.

 

Kulingana na Mbui, bunge lilikuwa likiwasukuma Wakenya kwenye kona hadi wakati mahakama zilipowaokoa kwa kusitisha utekelezwaji wa nyongeza ya ushuru wa mafuta.

 

Mbui amedokeza kuwa ilikuwa bahati mbaya kuona EPRA ikiongeza bei ya mafuta licha ya agizo la mahakama, jambo linaloonyesha wazi kuwa Kenya inaongozwa na serikali pinzani ambayo haijali raia wake wanaoteseka.

 

Alikuwa akizungumza wakati wa tafrija ya kustaafu ya mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Kathiani.

 

Mbunge huyo aliendelea na kuongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwa wajasiri wa kuitaka serikali na kuwatetea wanaowawakilisha Bungeni.
Wakati uo huo, aliwakemea waliopiga kura kuunga mkono Mswada wa Fedha bungeni, akisema kuwa wanawatendea dhuluma wapiga kura wao.

 

Aliongeza kuwa si haki kwa Wakenya kulipa zaidi kwani bidhaa zote zimeongezwa ilhali kuna pendekezo la kuongeza mishahara kwa maafisa wa serikali akiwemo Rais William Ruto na Naibu Rigathi Gachagua ili kuwakinga dhidi ya viwango vya ushuru vilivyoongezwa.

 

Agizo hilo la Mahakama lilitolewa baada ya Seneta wa Busia Okiya Omtatah kupinga Sheria ya Fedha, 2023 akitaka baadhi ya vipengele vya sheria hiyo kuondolewa.

 

Ongezeko hilo lililoanza Jumamosi usiku wa manane tayari limepandisha gharama ya usafiri huku wahusika wa sekta hiyo wakipanda bei za nauli.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!