Gachagua Ashangaza Umati Wa Watu
Naibu Rais Rigathi Gachagua Hii leo Jumatano alishangaza umati baada ya kudai Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alikuwa akiongea Kiingereza kupita kiasi.
Alipokuwa akizungumza katika mkutano wa maombi ya Kitaifa, Naibu Rais alimwambia Wetang’ula kwa mzaha aepuke kuzungumza Kiingereza sana kwenye hafla kama hizo.
“Spika wa Bunge, nashukuru kwa kunialika lakini wakati mwingine utakaponialika kwa hafla, naomba ufikirie upunguze kizungu kidogo, niweze kuelewa kile ambacho unasema” Gachagua alisema.
Wakati wa hotuba yake, Wetang’ula alimnukuu Rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela.
“Utukufu wa kweli wa kuishi haupo katika kujikwaa kamwe, bali katika kuinuka kila tunapoanguka.”
Alisema maridhiano yanaunganisha nchi pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa amani.
Aliwataka Wakenya kukumbatia roho ya upatanisho na Mungu na wanadamu wenzao.
Gachagua alisema mada ya mkutano huo wa Kitaifa wa mwaka huu ilikuja wakati ufaao huku Wakenya wakihitaji kusuluhu la ugumu wa maisha.
Alisema Rais William Ruto alikua Rais kwa sababu ya msamaha na maridhiano.
Wetang’ula alisema wanakusudia kuunganisha nchi.
“Upatanisho sio kazi rahisi kwani inatutaka kutazama ndani na kukubali mapungufu yetu,” alisema.