Home » DCI Kuchunguza Waziri Na Mbunge Mmoja

Waziri mmoja nchini pamoja na Mbunge wako kwenye chini ya uchunguzi wa idara ya Upelelezi na makosa ya Jinai (DCI) kuhusu kutoweka kwa sukari iliyokatiliwa na baadaye kupatikana masoko nchini.

 

Wawili hao ni miongoni mwa msururu wa washukiwa wanaodaiwa kushirikiana kuuza shehena hiyo ambayo tayari ilitangazwa kuwa si salama kwa matumizi ya binadamu mnamo mwaka wa 2018.

 

Ni wiki mbili tangu Shirika la Viwango nchini (KEBS) na maafisa kutoka DCI kugundua kuwa shehena hiyo ilikuwa imetoweka.

 

Juhudi za DCI za kutafuta shehena hiyo yenye sumu ya sukari zimeambulia patupu, huku hofu ikizidi kuwa tayari iko kwenye maduka makubwa kote nchini na wakenya tayari wameshatumia bidhaa hiyo.

 

Wapelelezi wa DCI wanaamini kuwa sukari hiyo tayari ilikuwa imepata muda wake hata kabla ya kutolewa katika Bandari ya Mombasa, na kwamba watu mashuhuri walikuwa nyuma ya mpango huo.

 

Wakenya wanaendelea kushangaa jinsi mifuko 20,000 ya sukari yenye sumu iliondoka Mombasa hadi kufika eneo la Makongeni, Thika, na kwa nini sukari hiyo iliyokatiliwa mwaka wa 2018 huenda tayari iko kwenye maduka makubwa.

 

Vinepack Industries mjini Thika ambapo sukari hiyo yenye sumu ilisemekana kuhifadhiwa ilipatikana katika mazingira tulivu huku kukiwa na mlinzi mmoja pekee anayesimamia biashara hiyo.

 

Hili lilikuwa jumba lile lile ambalo lilivamiwa na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) Septemba mwaka jana kwa shutuma za kufanya kazi bila leseni, kuzalisha pombe ghushi na kukwepa kulipa ushuru.

 

Maafisa wa DCI wako katika kinyang’anyiro cha kusuluhisha kitendawili cha shehena ya sukari iliyopotea tangu ilipoondoka Mombasa, ikiwa katika hali gani, jinsi ilivyotua na mahali ilipohifadhiwa kabla ya kutoweka.

 

Mnamo Aprili 12, 2023 timu ya mashirika mengi iliitwa kuratibu kutolewa kwa sukari iliyokatiliwa na KRA ambapo ilitakiwa kugeuzwa kuwa Ethanol kwa matumizi ya viwandani ilipofika Nairobi.

 

Aidha Siku iyo hiyo, mifuko yote 20,000 ya sukari iliyokatiliwa ilitumwa Thika kwa ajili ya kuratibiwa katika viwanda vya Vinepack.

 

Taarifa inafichua kuwa ilichukua siku 8 kushughulikia shehena hiyo katika Bandari ya Mombasa, kupeleka iyo hiyo hadi Thika na kushusha sukari ili kuhifadhiwa.

 

Mnamo Aprili 20, 2023, shehena hiyo ilipokelewa mjini Thika na timu ya mashirika mengi yenye makao yake makuu jijini Nairobi ambapo walishuhudia kufika kwa shehena hiyo.

 

Sasa inaibuka kuwa Vinepack iliipatia kampuni ya Kings Commodities Limited huko Thika kuhifadhi sukari hiyo.

 

Kulingana na barua ya KEBS kuhusu mchakato wa kubadilisha sukari hiyo kuwa ethanol, KEBS ilipaswa kuwepo pamoja na maafisa wa mamlaka ya mazingira NEMA ili kuhakikisha sukari yote inabadilishwa kuwa ethanol na sio kuelekezwa kwa matumizi mengine.

 

KEBS pia ilipaswa kuchukua sampuli za ethanol zinazozalishwa kwa ajili ya kuchunguzwa katika maabara zao zilizoidhinishwa, ili kuhakikisha kwamba inazingatia viwango vinavyohitajika.

 

Mnamo Mei 4, 2023 wakati maafisa wa KEBS, timu za mashirika mengi na DCI walirejea katika eneo la Thika kwa ajili ya mchakato, mifuko 20,000 ya sukari a ilikuwa imetoweka kwa njia ya ajabu.

 

Ni siku 14 sasa tangu sukari hiyo ambayo si salama kuripotiwa kupotea, huku wapelelezi bado hawajapata shehena hiyo; baadhi ya maafisa waliosimamishwa kazi wamerekodi taarifa na DCI kuhusu sakata hiyo ya sukari.

 

Katika kikao cha mgogoro kilichofanywa na KEBS jana Alhamisi, mvutano wa viongozi ulifanyika, Esther Ngari akiteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa miezi sita, huku Bernard Nguyo akiwa Kaimu Mkurugenzi mpya wa Uhakikisho wa Ubora na Ukaguzi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!