Uhuru Atuma Radhi Kwa Kukosa Mkutano Wa Azimio
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amekosa kushiriki mkutano wa Kundi la Wabunge wa muungano wa Azimio La Umoja One-Kenya huko Stoni Athi katika Kaunti ya Machakos.
Uhuru, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Azimio, hakuwa katika mkutano huo uliohudhuriwa na uongozi wa muungano huo miongoni mwao Raila Odinga, Martha Karua, na kundi la magavana kama vile Simba Arati, Gideon Mung’aro, Ochilo Ayako, James Orengo na Anyang Nyong’o.
Raila amesema Uhuru hata hivyo ameahidi kuunga mkono uamuzi wowote ambao wabunge wataafikia.
Mwenyekiti wa chama cha KANU Gideon Moi pia hakuwepo lakini ametuma radhi zake.
Raila amesema muungano huo unajiandaa kutuma wanachama wake kwa kamati ya bunge ya pande mbili, kulingana na makubaliano ya upinzani siku ya Jumapili kusitisha maandamano dhidi ya serikali na kushughulikia masuala yake na utawala wa Rais William Ruto.
Aidha, amesema pia watapendekeza sera na mageuzi ya kisheria ili kuboresha mchakato wa uchaguzi, na mapitio ya sheria ili kuhakikisha uamuzi wa chama unatiliwa maanani.