Wakili Ombeta Amwonya DJ Fatxo

Wakili maarufu wa Nairobi Cliff Ombeta amemuonya mwimbaji wa Mugithi DJ Fatxo kujiepusha na mahojiano na wanahabari.
Katika ujumbe wa Twitter, Ombeta amedai kuwa Fatxo ana hatari ya kujikanganya ikiwa ataendelea kuonekana kwenye vyombo vya habari kwa mahojiano kuhusu kifo cha Jeff Mwathi ambaye kila mkenya anafuatilia taarifa hiyo.
Wakili huo alisema kuwa chochote anachosema Fatxo hivi sasa ni hatari na kinaweza kutumika dhidi yake katika mahakama ya sheria na kmtaka Fatxo awaruhusu mawakili wake waongee wakati wote.
‘Acha kubabaika Unapaswa kuwa kimya wakati huu si wa kuongea chochote unachosema sasa ni hatari kwako waeza jikanganya Usiwape polisi sababu ya kupinga au kuchunguza Achia wakili uongee,” Cliff Ombeta
Lawrence Njuguna Wagura almaarufu DJ Fatxo anawakilishwa na Wakili Ndegwa Njiru na walikuwa pamoja wakati wa mahojiano na wahandishi wahabari siku ya Jumamosi.
Ushauri wa Ombeta unajiri wakati DJ Fatxo anakabiliwa na mzozo kuhusu mahojiano yake ya kwanza ya vyombo vya habari.
Siku ya Jumamosi, Fatxo alitoa maelezo mafupi kuhusu urafiki wake na marehemu Jeff Mwathi ambaye inasemekana alifariki nyumbani kwake.
Fatxo alisema kuwa alikuwa akimfahamu Jeff kwa miaka 2 na alikuwa akimuuzia viatu. Pia alitaja kuwa yeye ndiye aliyeripoti kuwa Jeff alipotea baada ya kufika nyumbani kwake na kumkosa siku ambayo inadaiwa Jeff alifariki jambo ambalo limeibua sintofahamu katika kauli zake.
“Baadaye nikirudi baada ya saa chache, nikakuta Jeff hayupo nyumbani mimi ndiye nilienda kituo cha polisi kutoa taarifa kuwa Jeff ametoweka.
“Pia kuna suala hili linaloendelea kwamba sikuomboleza kifo cha Jeff. Nilifikia. Mimi ndiye niliiambia familia kwamba Jeff hayupo tena.
“Kweli niliwasiliana nao na kuwaambia ningeweza kuwaunga mkono kumzika mtoto wao na tunakuja tukishirikiana.Ni jambo ambalo linaniuma pia. Kwa hiyo nilifikia hatua sikuwa napata majibu. Nikamwambia mama tafadhali unaweza kumpigia simu mmoja wa wanafamilia na kumuomba akubaliane na tushirkiane kwa ajili ya shughuli za mazishi.”
“Hili ni jambo jipya kwangu, hakuna namna naweza kumpoteza rafiki na kushindwa kumwomboleza. Labda mama Jeff hakuambiwa, labda hakuambiwa nataka tukutane lakini ninachotaka kusema ni kwamba tulifika,”.DJ FATSO.
Inadaiwa Mwathi alianguka kutoka orofa ya 10 ya Redwood Apartments kando ya barabara ya Thika anakoishi DJ huyo.
Mazingira ambayo alifariki bado hayajafahamika na DCI inachunguza kisa hicho.
Wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai, idara ya mauaji walitembelea nyumba ya DJ Fatxo siku ya Ijumaa na kwa sasa wanaendelea na uchunguzi.
Yakijiri hayo, kampuni mbili zimesitisha kandarasi na DJ Fatxo kama mabalozi wa chapa zao kwa sababu ya kifo cha kutatanisha cha Jeff Mwathi.
Mix master amedai kutokuwa na hatia katika kifo cha Mwathi lakini hii imefanya kidogo kuzuia kampuni kumkatiza.
Angalau kampuni mbili zimethibitisha kusitisha mikataba yao na DJ Fatxo hadi sasa.
Kampuni ya Lesedi Developers Ltd ilitangaza kukata uhusiano na DJ Fatxo kutokana na athari yake katika sakata ya kifo cha Jeff Mwathi.
Kampuni hiyo ya mali isiyohamishika katika taarifa ilisema kwa kuzingatia maadili yake, wameona ni vyema kujitenga na DJ Fatxo.